Ad imageAd image

Makatibu Wakuu wastaafu wapongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa bwawa la Julius Nyerere.

Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu Wastaafu waliowahi kuhudumu katika Wizara ya Nishati kwa nyakati tofauti wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Kiongozi wa Baraza la Mawaziri ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said wametembelea mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Electric Power Project – JNHPP) na kujionea maendeleo ya mradi huo ikiwa ni mwezi mmoja tokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan afunge rasmi lango la kuchepusha maji ya mto Rufiji ili kuruhusu maji kuanza kujaa ndani ya bwawa hili ambapo kwa sasa kina cha maji kwenye bwawa kimefikia urefu wa mita 116 kutoka usawa wa bahari.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mradi huo, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said ameeleza kuwa mradi huu ni mkubwa sana kwa Tanzania na hata nje ya Tanzania na unaendelea vizuri ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 80.22 na inategemewa hadi kufikia Januari 2024 umeme wa kwanza utaanza kuzalishwa na kusafirishwa hadi Chalinze ili uungwanishwe kwenye Gridi ya Taifa na hatimaye uweze kusambazwa kwenda sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Mhe. Mhandisi Zena ameeleza faida mbalimbali za mradi huu unaotarajiwa kuzalisha jumla ya megawati 2115 ikiwemo upatikanaji wa umeme wa uhakika ambao utaondoa kabisa changamoto ya upungufu wa umeme lakini pia vijana wengi walioshiriki katika ujenzi wa mradi huu watabakia na ujuzi utakaowawezesha kuweza kujiajiri na hata kutumika katika miradi mingine inayoendelea.

“Bwawa hili likimalizika kwa kweli litakuwa ni mkombozi mkubwa sana kwa sababu nchi yetu itaweza kupata umeme wa uhakika na kupelekea changamoto ya upungufu wa umeme kubaki historia kwa hiyo tuendelee kushirikiana ili tuweze kulikamilisha hili na baada ya hapa vijana wetu wengi watakuwa wamepata ujuzi kwa hiyo nitoe wito kwa Wizara ya Nishati waweze kuweka kanzidata ili kuwatambua wale wote waliohusika kwa sababu nimeambiwa asilimia 90 ya wafanyakazi ni watanzania” amesema Mhe. Mhandisi Zena.

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhe. Mhandisi Felchesi Mramba ameeleza kuwa, bwawa hilo litakuwa na faida nyingi kwa watanzania ambapo Serikali imeandaa mipango mingi ya matumizi ya bwawa hili ambayo ni pamoja na kutenga hekta laki nne kwenye Rufiji Delta ambazo zitatumika kwenye matumizi ya kilimo cha umwagiliaji lakini pia bwawa litatumika kwa ajili ya matumizi ya uvuvi na kuwezesha kupatikana kwa maji na umeme wa uhakika pamoja na kuwezesha ajira nyingi kwa watanzania.

Naye mmoja wa makatibu wakuu wastaafu, Dkt. Avemaria Semakafu ameipongeza Serikali na Wizara ya Nishati kwa kuuendeleza kwa kasi kubwa mradi huu wa kimkakati ambao unategemewa kuwa kichocheo cha maendeleo kwa watanzania na taifa kwa ujumla na kutoa wito kwa Wizara ya Nishati na TANESCO kuandaa Makala maalum itakayowahusisha wadau wote waliohusika katika kuanzishwa kwa mradi huu.

“Ningependa kuipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kuchukua mradi huu wa kimkakati lakini vilevile kwa kuuendeleza kwa kasi ambayo tunaiona, fedha iliyotumika ni nyingi sana lakini ni mategemeo yetu kwamba baada ya kukamilika na kuanza kutumika, mradi huu utachochea maendeleo kwa watanzania hasa ukielewa nishati ya umeme ni kitu cha msingi sana katika maendeleo hasa kwa taifa letu ambalo limefikia uchumi wa kati. Ombi langu kwa Wizara na kwa TANESCO watutengenezee Makala maalum itakayowahusisha wadau wote waliohusika kwenye ujenzi wa mradi huu.

Mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere Hydro Electric Power Project (JNHPP) unatarajiwa kuzalisha jumla ya megawati 2,115 zitakazoongeza nguvu katika megawati 1,600, zinazozalishwa kwenye vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme na kuondoa tatizo la umeme na kuiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa mahitaji ya umeme na kuwa na ziada ya kuuza nchi jirani sambamba na kupunguza gharama za umeme kwa Watanzania.

Share this Article
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

adbanner