Ad imageAd image

NMB Yakusanya Faida ya Bil. 429 kwa mwaka 2022

Na Rajabu Msangi

Benki ya NMB imeendelea kuunga mkono Serikari kwa kusaidia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kuboresha elimu, Afya, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia ya nchi kwa kutenga Shilingi Bilioni 6.2 kwa mwaka 2023 katika uwajibikaji kwenye jamii.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 26, Januari 2023 na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benk ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna wakati akiwasilisha Taarifa ya Fedha ya NMB kwa mwaka 2022 katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Serena jijini Dar es Salaam.

Bi. Ruth amesema Kwa mwaka 2022 Benki ya NMB imefanikiwa kupata faida baada ya kulipa kodi  na kufikia Bilioni 429 ambazo ni  sawa na asilimia 47 na kuongeza kuwa hadi saaa jumla ya mapato kufikia Trilioni 1.2.

“Faida baada ya kodi ya NMB imeongezeka kwa asilimia 47 na kufikia Shilingi Bilioni 429, Mwenyekiti wa Bodi, mwaka 2018 ambayo ni miaka minne kutoka hapa Benki ya NMB ilitengeneza faida baada ya kodi ya Bilioni 98, nayo tuliona ni mafanikio lakini miaka minne baadaye Benki hii inatengeneza faida ya Bilioni 429” Amesema Bi. Ruth.

Bi. Ruth  amesema mwaka 2022 ambao ulikuwa ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 25 ya Benki ya NMB jumla ya mapato ilifikia Bilioni 1.2

“Sanjari na nia yetu ya kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa kampuni mbalimbali, watu  binafsi lakini pia uwekezaji wetu ambao tunaendelea kuufanya hasa kilimo, biashara ndogondogo , za kati jumla ya mali ya hii Benki kwa sasa ipo Trilioni 10.2” Amesema Bi. Ruth.

Bi. Ruth ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayowezesha Benki ya NMB kupata mafanikio hayo ya kihistoria ni pamoja na ubora wa mpango mkakati na utekelezaji katika mipango inayoendeshwa na Benki hiyo.

Katika hatua nyingine amesema NMB imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 6.2 katika kuunga mkono serikali katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

“Kutokana na matokeo haya sisi Benki ya NMB sasa, tunatenga kiasi cha shilingi Bilioni 6.2 ili kusaidia jamii na kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania”

“Mheshimiwa Mwenyekiti kiasi hiki cha historia ni ongezeko la  zaidi ya asilimia 114 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Bilioni 2.9 ambazo tulizitenga na kutumika mwaka wa 2022, 2022 tulitenga Bilioni 2.9 ndo tulizipeleka kusaidia jamii katika maeneo mbalimbali” Ameongeza Bi. Ruth.

Katika suala la Elimu Benki ya NMB imesema kwa mwaka 2022 ilifanikiwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi 64 wa elimu ya juu nchi nzima.

“Ufadhili huu unajumuisha malipo ya ada, fedha za kujikimu, matibabu pamoja na manunuzi ya Kompyuta, Ufadhili huu unalenga watoto wetu wa kitanzania ambao wanatoka kwenye familia zenye uhitaji” Amesema Bi Ruth.

Aidha katika Sekta ya Afya NMB ilifanikiwa kutoa misaada mbalimbali katika vituo vya afya nchini ikiwemo vitanda, pamoja na vifaa tiba vingine.

“Tulitoa vitanda, tulitoa mashuka, tulitoa vifaa tiba vingine pamoja na vitanda vya kujifungulia kinamama kwa vituo zaidi ya 40 nchi nzima ,Tanzania Bara na Visiwani”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede amesema Benki ya  NMB inaahidi kuendelea kutoa huduma bora na zenye ubunifu kwa maslahi ya Watanzania, na kuisaidia serikali katika kuboresha huduma za kijamii.

Share this Article
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

adbanner