Ad imageAd image

JICA na UDSM kufanya jambo hili kubwa,waja na mdahalo kabambe

Na Yusuph Digossi

IMEELEZWA kuwa uhusiano  uliaoasisiwa mnamo mwaka 1962 kati ya mataifa ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) yanatazamiwa kuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo Uchumi pamoja na kijamii.

Katika kuthibitisha tija kwenye mahusiano hayo Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamepata heshima ya kuanda mdahalo wa siku mbili ambao unahusu masuala ya Uvumbuzi ambayo ni sehemu kubwa ya majukumu ya Chuo hicho katika ufundishaji na ujifunzaji, utafiti na ubunifu na utoaji huduma kwa jamii.

Mkurugenzi, Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo (UDSM), Salvatory Nyanto (PhD)amewaambia wanahabari leo jijini Dar es salaam kuwa faraja kwao kufanya midahalo kama hiyo ili kufikia jamii ya Watanzania kwa urahisi na kutatua changamoto zao mbalimbali kupitia utafiti, majadiliano, ufundishaji na ujifunzaji.

“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni Chuo kikongwe nchini Tanzania, mwaka jana (2022) kiliadhimisha miaka 60 ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti, ubunifu na utoaji huduma kwa jamii,” amesema Dkt. Nyanto.

Aidha,Dkt. Nyanto ameongeza: “Kama ilivyo kwa Shirika la JICA mwaka 2022 walitimiza miaka 60 ya utoaji huduma hapa Tanzania, ushirikiano huu unasaidia maendeleo vijijini lakini pia kusaidia kufikia malengo ya Serikali ya Tanzania kuhudumia Wananchi wake.”

Amesema mdahalo huo ni fursa tosha kwa Chuo Kikuu (UDSM) na Wanajumuiya ya Chuo hicho sanjari na Watanzania kwa ujumla kutumia nafasi hiyo kujifunza, kujadili masuala ya uvumbuzi yavyochangia maendeleo, pamoja na kujadili masuala ya ujasiriamali.

Vilevile,Dkt. Nyanto amesema mdahalo huo utaangazia zaidi dira ya mwaka 2061 ya Chuo hicho Kikuu, ambayo inajikita katika kuongeza masuala ya mashirikiano ya kitaaluma, kuongeza wigo wa mataifishaji pamoja na kuongeza wigo wa ufundishaji, ujifunzaji na uvumbuzi.

Naye, Mwakilishi Mkuu wa Shirika la JICA nchini Tanzania, Yamamura Naofumi amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya shughuli mbalimbali za JICA nchini na pia kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa UDSM, JICA kwa kushirikiana na UDSM wameshariki kuandaa hafla chini ya “Programu ya JICA kwa Mafunzo ya Kijapani” iitwayo. ‘Japan – Tanzania Innovation Forum’ na mada kuu ya Jukwaa hilo itakuwa: Ubunifu kwa Ukuaji wa Taifa na Maendeleo Endelevu.

Amesema JICA na UDSM waliamua kuchagua mada hiyo baada ya mashauriano ya kina na wadau mbalimbali, “Jukwaa linatarajiwa kuja na majibu ya wazi kwa maswali kama vile: Je, Tanzania inapaswa kufanya nini ili kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo katika ubunifu kwa ukuaji na maendeleo ya taifa?,” amesema Yamamura

“Je, kuna changamoto gani katika kukuza ubunifu, hasa miongoni mwa vijana nchini Tanzania?, Kwa kuzingatia uhusiano wetu wa miaka 60 iliyopita, je Japan na Tanzania zinawezaje kushirikiana zaidi kupitia Ubunifu katika siku zijazo?”

Mdahalo huo wa siku mbili utafanyika Februari 9 na 10, 2023 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maktaba Kuu na utashirikisha Wanajopo mbalimbali wakiwemo Wataalamu mbalimbali kutoka nchi hizo mbili, Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wahadhiri kutoka Vyuo vikuu nchini Japan.

Share this Article
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

adbanner