Ad imageAd image

Tanzania na Benki ya Dunia zasaini Mkopo Nafuu kuboresha Huduma za afya

Serikali ya Tanzania na Banki kuu ya Dunia zimesaini mkopo nafuu utakaosaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuboresha huduma za dharura, kuboresha rasilimali watu katika Sekta ya afya, kuboresha utendaji na ufanisi kwenye ngazi ya zahanati.

Hafla hiyo fupi imeongozwa na Waziri wa fedha na mipango nchini Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya bara Dkt. Godwin Mollel aliyemwakilisha Waziri wa Afya pamoja na mwakilishi kutoka Serikali ya Zanzibar Mhe. Amur Mohamed na viongozi wengine kutoka Wizara ya fedha, Maji na Wizara ya Afya.

Dkt. Mwigulu amesema, mpango huu nafuu, ni mwendelezo wa miradi iliyopita ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi ikiwemo kuboresha afya ya mama na mtoto hususan huduma katika ngazi ya zahanati ambapo idadi kubwa ya wananchi huenda kupata huduma.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, Wizara ya afya kwa kushirikiana na OR TAMISEMI kuanza kutekeleza mkakati huu wa kupambana dhidi ya vifo vya mama na mtoto kuanzia mwezi Machi 2023 mpaka mwezi Desemba 2027 ambapo dola za Kimarekani milioni 250 kama mkopo nafuu na mkopo nafuu wa dola za kimarekani milioni 25 kutoka Global facility financing.

Amesema, Dola za Marekani milioni 244 zilitolewa na Banki kuu ya Dunia kupitia mpango harakishi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 katika vizazi hai 100,000 (TDHS 2015) mpaka vifo 238 katika vizazi hai 100,000 (WHO 2023).

Aidha, Dkt. Mollel ameeleza vifo vya watoto vimepungua kutoka 67 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2021) mpaka 43 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2022) sawa na asilimia 35%, ingawa hali hiyo haifanani kwenye kwa vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa, ambayo inaonesha kushuka kutoka vifo 25 kwa vizazi hai 1,000 (TDHS 2015) mpaka vifo 24 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2022).

Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, Sekta ya afya inaendelea kutekeleza mkakati harakishi ili kufikia malengo ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi mpaka kufikia vifo 100 katika vizazi hai 100,000, na kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa 15 katika vizazi hai 1,000 mpaka kufikia mwaka 2025.

Share this Article
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

adbanner