







Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kimesaini mikataba ya utekelezaji na miradi kumi ya kimkakati inayotekeleza miradi kwenye sekta mbalimbali hapa nchini ambayo inatarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini hapa nchini .
Akiongea baada ya zoezi la kusaini makubaliano hayo waziri wa Uwekezaji viwanda na biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kusainiwa kwa mikataba hii ni uthibitisho kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kukuza uchumi kupitia uwekezaji na kuzitaka Taasisi zote zinazotoa huduma kutoa ushirikiano kwa wawekzaji ili kuhakikisha mikataba ya wawekezaji hao inatekelezwa kwa wakati.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Gilead Teri amesema hii ni mara ya kwanza kwa TIC kusaini mikataba 10 kwa wakati mmoja ambapo miradi hiyo kwa pamoja inathamani ya dola za kimarekani 1805.15 na inatarajiwa kuleta ajira zipatazo 16355 na ajira 244400 zisizokuwa za moja kwa moja.
Miradi hiyo Kumi ya kimkakati na Mahiri ambayo mesaini mikataba ya utekelezaji na TIC leo ni kama ifuatavyo;
- Mradi wa kwanza ni mradi wa kongani ya Viwanda wa Sinotan unaotekelezwa Kwala Mkoani Pwani
Mradi huu ni wa Kongani ya viwanda na unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuwa na viwanda Zaidi ya 200 ndani ya mradi mara utakapokamilika. Mradi utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 327 milioni na kuleta ajira zipatazo 2000 za moja kwa moja na 50,000 ambazo si za moja kwa moja.
- Mradi wa Kilombero Sugar unaotekelezwa Mkoani Morogoro
Mradi huu ni wa upanuzi wa Kilimo cha Miwa na Kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 238.5 milioni na kuleta ajira mpya zipatazo 1404 za moja kwa moja na 15,000 ambazo si za moja kwa moja. Kiwanda baada ya upanuzi kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 271,000 za sukari na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji sukari kutoka nje.
- Mradi wa WILMAR unaotekelezwa Kihonda Morogoro
Mradi huu ni wa viwanda na uchakati wa nafaka na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 51.5 milioni na kuleta ajira mpya zipatazo 360 za moja kwa moja na 1,000 ambazo si za moja kwa moja. Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 271,000 za mchele na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji mchele kutoka nje na kutakuwa na vituo 38 vya kupokea nafaka ya mpunga kutoka kwa wakulima na hivyo kuongeza soko kwa wakulima wetu. Mradi utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuchakata tani 1,150 za mpunga kwa siku na kuingizia Taifa takribani dola milioni 50 kwa mwaka kutokana na mauzo ya bidhaa hiyo nje ya nchi.
- Mradi wa Upanuzi wa kiwanda cha uzalishaji wa saruji wa Lake Cement unaotekelezwa Kigamboni Dar-es-salaam
Hadi sasa mradi huu umewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 101. Mwekezaji anapanga kupanua kiwanda kwa kuwekeza mtaji mpya wa Dola za Kimarekani Milioni 26 na kufanya mradi kuwa na jumla ya Dola za Marekani Milioni 127. Mradi unatoa ajira za moja kwa moja 401 na ajira zisizo za moja kwa moja kufikia 450 Mradi utakapokamilika baada ya upanuzi uzalishaji utaongezeka kufikia Tani 1,000,000 kwa mwaka.
- Mradi wa kusindika na kuhifadhi Gas ya LPG
na miundombinu ya Gas wa Oilcom unaotekelezwa Dar-es-salaam
Mradi huu ni wa uchakataji wa Gesi na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 111.87 milioni na kuleta ajira zipatazo 1600 za moja kwa moja 160,000 zitakazotokana na mnyororo wa thamani wa mradi huo.
Mradi unatarajia kuwa na uwezo wa kupokea na kuhifadhi kiasi cha tani 15,000 za gas na hivyo kuongeza uwezo wa Taifa wa miundombinu ya uhifadhi gas na Kuwezesha Taasisi mbalimbali kama mashule, vyuo, kambi za Jeshi, Hospitali, Mahoteli na kadhalika kupunguza gharama za nishati na kulinda mazingira kwa kutumia nishati safi na rafiki wa mazingira.
- Mradi wa Wild Flower and Oil Mills unaotekelezwa Manguanyuki Singida
Mradi huu ni wa Kiwanda cha usindikaji wa mafutta ya kula utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 24 milioni na kuleta ajira zipatazo 190 za moja kwa moja na 400 ambazo si za moja kwa moja. Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 75 kwa siku za mafuta na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji mafuta kutoka nje.
- Mradi wa Mufindi Paper Mills unaotekelezwa Mkoani Kigoma
Mradi huu ni wa Kilimo cha Miwa na Kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 320 milioni na kuleta ajira mpya zipatazo 3000 za moja kwa moja na 2000 ambazo si za moja kwa moja. Kiwanda baada ya kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 340,000 za sukari na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji sukari kutoka nje.
- Mradi wa Lodhia Steel unaotekelezwa Mkuranga Mkoani Pwani
Mradi huu ni wa Kiwanda cha uzalishaji wa mabati utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 45 milioni na kuleta ajira zipatazo 400 za moja kwa moja na 150 ambazo si za moja kwa moja. Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 140,000 za mabati kwa mwaka.
- Miradi ya Dangote Cement unaotekelezwa Mkoani Mtwara
Na 10. Ni Mradi wa Mount Meru Millers unaotekelezwa Mkoani Singida
Miradi hii miwili ya Dangote Cement na Mount Meru Millers ni miradi ambayo tayari ilipewa hadhi ya Uwekezaji mahiri na leo tutashuhudia ikisaini mikataba ya makubaliano ya utekelezaji ya nyngeza.